JOHN TENDWA AZUNGUMZIA KWA VYAMA VYA SIASA



OFISI  ya Msajili  wa  Vyama Vya Siasa  nchini imevitaka  vyama vya siasa kutii agizo la kutoanzisha kambi za mafunzo ya kulinda amani maarufu kwa jina la mgambo , huku ikisisitiza kwamba itachukua hatua za kisheria  kwa chama chochote kitakachoiuka , ikiwemo kukifuta.

Aidha ofisi hiyo imesema kuwa  Katiba ya nchi imempa jukumu  kila mwananchi kulinda amani na usalama wa nchi, pia kujilinda yeye mwenyewe na mali zake kwa kutoa taarifa katika vyombo vya dola pale anaposikia au kuona mtu anataka kufanya au anafanya uhalifu au amemdhuru mtu.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dares Salaam na ofisi hiyo katika taarifa yake iliyoitoa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Rajab Juma kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa kufutia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza hivi  karibuni kinakusudia kuanzisha kambi za mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.

Alisema suala hilo lilitangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kuandikwa katika vyombo vya habari kabla ya chama hicho, kuwasiliana na taasisi  husika ikiwemo ofisi hiyo ili kupata ushauri kuwa 



 jambo wanalotaka kufanya ni sahihi.

“Hivyo Katiba ya nchi  na katiba za  za vyama vya siasa, hazina maana kila mwananchi au kikundi fulani wafanye mafunzo ya kijeshi au ukakamavu ili kufanikisha jukumu hili.

 “Jukumu la vikundi kama hivi ni kutoa taarifa kwa vyombo vya dola na si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru wenye jukumu la kupambana na wahalifu ni vyombo  vya ulinzi na usalama ambavyo vipo kisheria, mojawapo ikiwa ni Jeshi la Polisi,” alisema  Juma.

Juma alikitaka  chama hicho na vyama vingine vinavyofikiria  au kufanya jambo hilo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kukiuka Sheria za Nchi ikiwemo  Sheria ya Vyama  Vya  Siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 9(2)(C) cha sheria hiyo  kinakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika, kushabikia au kutumia nguvu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa.

Alisema chama cha siasa kutoa mafunzo ya kutumia nguvu kwa wanachama wake, ili kutekeleza jambo lolote lile ikiwamo kujilinda ni mojawapo ya masuala yanayokatazwa  na Sheria  ya Vyama vya Siasa.

Aliongeza kuwa kifungu cha (20) cha Sheria ya Vyama Vya Siasa kinasema uamuzi wa Msajili ni wa mwisho na hauwezi kukatiwa rufaa mahakamani.

Akizungumzia kuhusu madai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  wana kambi za mafunzo ya kupambana na vijana wake kama kisingizio cha kuvunja sheria hiyo alisema hayana msingi.

“Kama CCM  wanakiuka sheria ni jukumu la CHADEMA, kila Chama na kila Mtanzania, kutoa taarifa na ikiwezekana na ushahidi katika taasisi husika, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa  Vyama Vya Siasa ili suala hili lishughulikiwe kisheria,” alisisitiza.

Msajili   huyo aliviasa vyama vya siasa kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa ili kuchangia maendeleo ya nchi, badala ya kutumia uwezo wao na muda wa kubuni mambo yanayoleta mtafaruku na kuhatarisha mani na utulivu wa nchi yetu.

“Amani   ikitoweka vyama vya siasa vitakuwa katika makaratasi tu. Kutakuwa  hakuna mikutano wa kamati kuu, hakuna ‘press conference’ yaani mikutano na waandishi wa habari, hakuna operesheni ya kuzunguka nchi nzima n.k. Demokrasia hutekelezwa na kukua mahali penye amani na utulivu,” alisema

No comments:

Post a Comment