AFYA YA MAALIM NGURUMO YAZIDI KUDHOHOFIKA...MARADHI YA MWILI YADAIWA KUMTESA SANA...!!

KILA binadamu hutamani kuwa na mwisho mzuri. Hakuna apendaye kupatwa na misukosuko ya kiafya, awe dhaifu hata kushindwa kutoka ndani angalau akajitafutie riziki.

Waja hupanga na kupangua tu lakini mwamuzi wa leo na kesho ni Mungu aliye juu! Tafakari leo upo vema, una siha njema, tena barabara kabisa. Ikifika nyakati upo ndani huwezi kutoka itakuwaje? Usimcheke anayelia leo, hujui kesho yako itakuwaje.
Muhidin Maalim Gurumo, 72, alipata kuwa mwanaume shupavu sana. Mungu akamjalia kipaji cha muziki, akabarikiwa nyota ya kupendwa. Asimamapo jukwaani basi mashabiki ni hoihoi na raha tupu.

Tangu miaka ya 1960 kama ungethubutu kutamka humjui Gurumo, ungeonekana mshamba mwenye tongotongo nyingi, mjini ungechekwa. Alikuwa staa mkubwa sana wa muziki. Jina lake limebaki juu kuanzia nyakati hizo mpaka sasa.
Ni kamanda hodari, aliyeifanya Bendi ya Msondo ‘Msondo Ngoma’ ipate heshima kubwa mpaka ikaitwa Baba ya Muziki Tanzania. Tungo zake nyingi ni lulu ambayo haitafutika kamwe. Kinachoumiza kwa sasa ni kuona Gurumo hawezi tena kusimama jukwaani.
Hana uwezo wa kutoa burudani iliyozoeleka. Ile sauti yake yenye mawimbi haipatikani tena katika majukwaa ya muziki. Kikubwa kinachotesa moyo ni kwamba Msondo ambayo ni bendi yake, akimiliki hisa za kutosha kama mmoja wa wamiliki, haina msaada wowote kwake.
Mzee analalamika. Msondo hii ndiyo ile aliyoivusha kupitia majina ya Nuta, Juwata, na Ottu, ikiwa inamilikiwa na Chama cha Wafanyakazi. Hakujua kama mambo yangekuwa hivi leo.
Itambulike kuwa yeye akiwa na wenzake kama marehemu Shaaban Mhoja Kishiwa maarufu kama ‘TX Moshi William’, Saidi Mabera, marehemu Suleiman Mbwembwe, Othuman Momba, Joseph Maina na wengineo, ndiyo waliounganisha nguvu na kuimiliki, baada ya chama cha wafanyakazi kujiondoa katika uendeshaji wa bendi.
Mzee analia ukata. Maradhi yanamtesa lakini shida za dunia na msongo wa mawazo ambao anao kutokana na kutengwa na wenzake, ni hatari kubwa inayofupisha siku zake za kuishi.

ANAUMWA NINI? ALIANZA KUUMWA LII?
Katika mahojiano na mwandishi wetu, nyumbani kwake, Ubungo Garage, Dar es Salaam, Gurumo anasema: “Ninasumbuliwa na maradhi ya moyo. Nakumbuka nilianza kuumwa yapata miaka mitatu iliyopita. Kipindi hicho ndipo nilipatwa matatizo ya kushindwa kuimba kwa sauti ya juu.
“Kila nilipojitahidi kuimba kwa sauti ya juu, nilijikuta nikichoka sana. Niliendelea kujikaza lakini siku moja nilizidiwa, nikapelekwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
“Hospitali walinipima kwa kina, wakagundua moyo wangu umepanuka, yaani umekuwa mkubwa kuliko kipimo chake cha kawaida. Madaktari wakanishauri nipumzike kwa muda, niache kuimba. Nikatii ushauri.”
AJITUTUMUA NA KURUDI JUKWAANI
“Naipenda sana kazi yangu ya muziki. Vilevile kazi yangu ndiyo iliyokuwa inaniwezesha kupata fedha za kujikimu, kwa hiyo baada ya kujiona nina nafuu kidogo nilirudi jukwaani.
“Niliporudi kazini nilikuwa naimba lakini siyo sana kama mwanzoni. Mashabiki wangu waliponiona nimerudi, walifurahi sana, hivyo kuzidi kunipa moyo. Hata hivyo, hali yangu ikawa siyo nzuri kadiri siku zilivyosogea, mwisho daktari akanishauri niache kabisa kuimba.”
MATESO YA KULIPA KISOGO JUKWAA
“Kwa sasa nateseka sana. Muziki umekuwa kila kitu kwangu kwa takriban miaka 50 sasa. Ni kazi ambayo nimeifanya kwa moyo wangu wote katika kipindi chote hicho. Leo hii ugonjwa unanilazimisha nisiimbe.
“Pamoja na kuumia lakini sina jinsi, siwezi kulazimisha kupanda jukwaani kuimba kwa sababu hali itakuwa mbaya zaidi. Kuna wakati nikiwa ndani, nikisikiliza nyimbo zangu, machozi yananitoka, siamini kwamba kila kitu kwenye maisha yangu kimebadilika.’
MBONA MSONDO HAWAMTHAMINI?
Gurumo ni mmoja wakurugenzi wa Msondo lakini analalamika: “Ni jambo la kusikitisha sana, unajua Msondo ni yetu sote, mimi nikiwa mmoja wa wamiliki, nastahili mgawo kulingana na jinsi bendi inavyoingiza lakini toka niugue, sijawahi kupata chochote.
“Kuna kipindi mwanamuziki mmojammoja anajitoa na kunisaidia alichonacho lakini siyo fungu linalotokana na mgawo ambalo kwa hakika nastahili. Pamoja na hivyo, namshukuru Mungu kwa yote.
“Nimetumikia Msondo kwa muda mrefu sana na nilipata ugonjwa huu nikiwa kazini. Hata nilipoanza kuugua bado niliendelea kuimba. Nimefanya kazi kwa uaminifu wangu wote. Ingefaa wakathamini mchango wangu, kile wanachokipata nami wanikumbuke.”
ANGALAU NYUMBA INAMSITIRI
“Kwa kweli kitu ambacho naweza kujivunia sana ni nyumba yangu hii niliyoijenga mwaka 1984, kipindi hicho nilikuwa Bendi ya Mlimani Park Orchestra, kipindi hicho ikiitwa DDC Mlimani Park Orchestra.
“Kama siyo nyumba hiyo sijui leo ningekuwa mgeni wa nani. Fikiria kuwa leo hii siwezi kufanya kazi, ningepata wapi fedha za kulipa kodi? Labda ningerudi kijijini ambako huko mateso yangekuwa makubwa zaidi kutokana na haya maradhi yangu.”
FARAJA PEKEE NI MKEWE
“Japokuwa naumwa lakini hakuna kitu kinachonipa faraja kama mke wangu, Pili Said. Nimeishi naye tangu mwaka 1967, haikuwahi kutokea kufikiria kuongeza mke mwigine.
“Tumezeeka pamoja, siku zote tumeishi kwa upendo na maelewano sana. Nazidi kumshukuru kwamba kipindi hiki naumwa, yeye ndiye faraja yangu ya pekee.”
AIOMBA SERIKALI IMSAIDIE
“Nikiwa kama mwanamuziki wa muda mrefu sana, naomba serikali inisaidie. Nilijituma muda mrefu jukwaani, kwa hiyo naomba nithaminiwe, kwani sasa hivi sipati mahitaji muhimu.
“Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete kwa kuja kuniona kipindi nilipokuwa nimelazwa Muhimbili, siku ile nilijiona mwenye bahati sana kutembelewa kiongozi huyo mkuu wa nchi, alinifariji sana.”
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
“Nilizaliwa Masaki, Wilaya ya Kisarawe, Pwani, mwaka 1941. Elimu ya Msingi ilisoma Shule ya Pugu kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu, mwaka 1956, mjomba wangu alinihamishia Dar es Salaam ambako nilisoma zaidi masomo ya Kuran, Mtaa wa Lindi, Ilala.
“Nilisoma Kuran mpaka mwaka 1960 ambako nilijiunga na Nuta. Mwaka 1967, nilifuga ndoa na mke wangu, hivyo kufanikiwa kuzaa watoto wanne.
“Bendi ya Nuta baadaye ilibadili jina na kuitwa Juwata, baadaye Ottu Jazz. Mwaka 1978 nilihamia Mlimani Park Orchestra na mwaka 1985 nilijiunga na Bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS- Ndekule) lakini siku zote maisha yangu yamekuwa Msondo ambayo ndiyo bendi iliyopitia majina ya Nuta, Juwata na Ottu.”
Mwaka 1990 Gurumo pamoja na mwimbaji Hassan Rehan Bitchuka walirudi Msondo na tangu hapo mwimbaji huyo hajaihama bendi hiyo mpaka anaposumbuliwa na maradhi ingawaje swahiba wake mkubwa Bitchuka alirudi Mlimani Park mwaka 2002.
WENZAKE MSONDO WANASEMAJE?
Mmoja wa wakurugenzi wa Msondo, Saidi Mabera anatoa maelezo yanayopingana na Gurumo, anasema: “Ninachojua ni kwamba kile ninachopata mimi ndicho ambacho Gurumo anakipata. Kama hakimfikii hapo mimi sina la kusema.”
USHAURI
Hili suala la Gurumo kutengwa na wenzake inafaa liangaliwe kwa makini sana. Msondo wanatakiwa kumjali mwenzao. Mabera fanyia kazi hili, kama mgawo unatoka, sasa inakuwaje haumfikii?

No comments:

Post a Comment