SERIKALI YAANZA KUJENGA KIWANDA CHA GESI MTWARA...



Rais Jakaya Kikwete akiangalia shughuli za uzalishaji umeme hivi karibuni, baada ya vutanikuvute ya muda mrewfu Serikali imeamua kujenga kiwanda cha gesi mkoani Mtwara 

Na Editha Majura, Mwananchi


HATIMAYE ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi kabla ya kusafirishwa kwenda Dar es Salaam umeanza mkoani Mtwara. 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alisema jana kuwa ujenzi huo unaofanywa na Kampuni ya China Petroleum and Technology Development Co-operation (CPTDC), ambao awali, ulipaswa kuanza wiki iliyopita, umeanza juzi baada ya Serikali kufikia mwafaka na wananchi wa Kijiji cha Msimbati kinapojengwa. 



“Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (Wilman Ndile) na vijana wake walilazimika kufika Kijiji cha Msimbati, ambako wananchi walikuwa na mgogoro na watu wa Marine Park,” alisema Maswi. 


Alisema baada ya ziara hiyo kushindwa kufanyika Jumapili iliyopita, uongozi wa wilaya ulikutana na viongozi wa kijiji na kufikia mwafaka uliofanikisha kuanza kwa ujenzi huo. 


Alisema kuanzia mradi huo kutatoa ajira za kawaida kwa wakazi saba wa maeneo yanayozunguka mradi huo na kwamba kazi hiyo itaongeza mahitaji ya bidhaa mbalimbali na huduma katika Kata ya Msimbati 


“Mathalan kuku, matunda na mboga za majani vinahitajika sana. Sasa wananchi ambao awali, hawakutaka kuelezwa lolote, wameanza kuchangamkia fursa hizo jambo ambalo litawanufaisha zaidi,” alisema. 


Ujenzi huo ulielezwa kuwa unatekelezwa sambamba na mwekezaji kujenga visima vitatu vya maji safi na salama kijijini Madimba. 


Alisema mwekezaji pia atasambaza umeme kwa kaya 300 za ndani na jirani ya kijiji hicho na kwamba vifaa vitakavyotumika katika kazi hiyo vinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu. 


Maswi alisema shule zote kwenye Kata ya Msimbati kikiwamo Kijiji cha Madimba, zitakarabatiwa na mwekezaji huyo ikiwa ni sehemu ya mpango wa wananchi waishio maeneo ya mradi kunufaika na uwekezaji. 


Hata hivyo, habari nyingine zinaeleza kuwa ulinzi umeimarishwa katika eneo hilo la mradi ili kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuwapo. 


Mgawo wa umeme
Akizungumzia kuhusu kukatika mara kwa mara kwa umeme katika maeneo mengi nchini hali inayowafanya wananchi kuamini kuwa kuna mgawo wa umeme kinyemela, Maswi alisema kamwe Taifa halitaingia gizani. 


Alisema kukatika kunakotokea sasa kumesababishwa na kazi za kiufundi zilizotarajiwa kukamilika jana jioni... “Kwa taarifa nilizonazo, mtambo mdogo uliopo Ubungo unabadilishwa na kuwekwa mkubwa, pia Kipawa kuna matengenezo ya transfoma ili kuwezesha usambazaji wa umeme hadi Kisarawe na nyie mnaweza kwenda mkashuhudia kinachoendelea.” 


Hata hivyo, taarifa kutoka Mikoa ya Kilimanjaro, Dodoma, Morogoro, Arusha na Mwanza zinasema kumekuwa na tatizo kubwa la umeme kwa wiki mbili sasa.

No comments:

Post a Comment